2

Sikukuu ya jamaa
1 Basi niliporejea nyumbani kwangu na kupatiwa tena mke wangu Ana na mwanangu Tobia, niliandaliwa karamu kubwa wakati wa sikukuu ya Pentekoste, iliyo sikukuu takatifu ya majuma saba. Nilipokuwa nimekaa mezani na kuona vyakula vingi mezani,
2 nikamwambia Tobia, “Mwanangu, nenda nje ukaangalie kama kuna maskini Myahudi mwenzetu mcha Mungu, umlete hapa. Haya! Nakungojea.”

Mauaji mjini Ninewi
3 Basi, Tobia akarudi na habari hii: “Baba! Kuna mtu mmoja wa taifa letu amenyongwa, akatupwa sokoni!”
4 Papo hapo, hata bila kuonja chakula changu, niliondoka kwa haraka nikamchukua huyo maiti kumficha kibandani ili nimzike saa za jioni.
5 Kisha nilirudi nyumbani, nikaoga, nikala chakula changu kwa majonzi.
6 Nikakumbuka maneno ya nabii Amosi: “Sikukuu zenu zitageuka kuwa maombolezo, na nyimbo zenu kilio.” Nami sikuweza kuyazuia machozi yangu.
7 Jua lilipotua nilitoka nje, nikachimba kaburi na kumzika marehemu.
8 Lakini jirani zangu wakanidhihaki wakisema, “Mtazameni huyu! Haogopi tena! Safari ile alinusurika kuuawa kwa sababu ya kufanya hayohayo. Bahati yake alichopoka. Lakini sasa anarudia mambo yaleyale!”

Tobiti apofuka
9 Jioni hiyo nilirudi nikaoga; kisha nikaenda kulala nje uani, kando ya ukuta. Kwa kuwa kulikuwa na joto sana sikujifunika uso.
10 Wala sikujua ya kwamba kulikuwapo mbayuwayu ukutani juu yangu. Basi wakanidondoshea machoni mavi yao yenye moto, vigamba vyeupe vikaziba macho yangu. Niliwaendea waganga mbalimbali, lakini hakuna aliyeweza kuniponya; mwisho nikawa kipofu kabisa. Kwa miaka minne sikuweza kuona chochote. Ndugu zangu walinishughulikia sana, na Ahika alinitunza kwa miaka miwili, kisha akaenda zake nchini Elamu.
11 Wakati huo ikambidi mke wangu Ana kufanya kibarua: Kufuma nguo, kama wanawake wengine.
12 Mara kwa mara aliwapelekea waajiri wake nguo alizotengeneza. Siku moja, baada ya kumlipa ujira wake walimzawadisha mwanambuzi.
13 Ana alipowasili nyumbani, mwanambuzi huyo akaanza kulia. Mimi nikamwuliza mke wangu, “Mbuzi huyo ametoka wapi? Umemwiba sivyo? Mrudishe kwa mwenyewe! Si halali kula vitu vilivyoibiwa!”
14 Ana akaniambia: “Sivyo! Huyu mwanambuzi nimepewa zawadi pamoja na mshahara wangu.” Lakini mimi sikumwamini; nikaona haya kwa kitendo hicho alichofanya. Nilimwamuru amrudishe huyo mbuzi kwa wenyewe. Ndipo aliponijibu: “Haya basi! Wewe uliwasaidia maskini au sivyo? Matendo yako yamekupatia nini? Yaliyokupata ni dhahiri!”

Generic placeholder image