6

1 Basi, Ana akaacha kulia.

Tobia akamata samaki
Hapo, Tobia akifuatwa na mbwa wake, akaanza safari pamoja na yule malaika. Jioni ya siku ile ya kwanza ya safari wakawa wamefika kando ya mto Tigri.
2 Basi, kijana Tobia akateremka mtoni kunawa miguu. Mara, samaki mkubwa akaruka kutoka majini, akataka kummeza Tobia. Kijana alipiga ukelele,
3 naye malaika akamwambia: “Mkamate huyo samaki! Usimwachilie!”
4 Kijana akamkamata samaki na kumvutia nchi kavu. Malaika akasema, “Mpasue samaki huyo, utoe nyongo, moyo na ini lake, uviweke pembeni; lakini matumbo yatupe. Hiyo nyongo yake, moyo na ini lake vinafaa kwa dawa.”
5 Tobia akafanya kama malaika alivyokuwa amemwambia. Halafu akakaanga sehemu moja ya huyo samaki kwa chakula na sehemu nyingine akaitia chumvi kuihifadhi. Basi wakaendelea na safari yao pamoja mpaka walipokaribia Media.
6 Hapo Tobia akamwuliza yule Malaika, “Ndugu Azaria! Je, hiyo nyongo ya samaki, ini na moyo vyaweza kuponya magonjwa gani?”
7 Malaika akajibu, “Moyo huo na ini unaweza kuvichoma motoni na kutumia moshi wake kufukuzia jini au pepo mbaya anayemsumbua mtu. Usumbufu huo utatoweka kabisa bila kuacha hata alama yake.
8 Na hiyo nyongo hutumiwa kumpaka mtu yeyote aliye na vigamba vyeupe machoni, naye hupona.”

Njiani kwenda Ekbatana
9 Walipokuwa wamefika nchini Media, karibu na mji wa Ekbatana,
10 Rafaeli akasema, “Ndugu yangu Tobia!” Tobia akaitika “Naam!” Malaika akaendelea kusema, “Leo usiku tutakaa na Ragueli ambaye ni wa jamaa yako. Yeye ana mtoto mmoja tu wa kike, aitwaye Sara.
11 Kimila wewe ni wa karibu sana naye na unayo haki ya kumwoa Sara na kurithi mali ya baba yake.
12 Sara ni binti mwenye busara, hodari na mzuri sana na baba yake anampenda sana. Usiku huu nitaongea na baba yake akubali umpose Sara. Halafu, tutakaporudi nyumbani kutoka mjini Rage, tutasherehekea harusi yako. Ragueli hawezi kukukatalia kumwoa Sara, wala hawezi kumruhusu mwanamume mwingine amwoe. Kama atamruhusu mwanamume mwingine amwoe atakuwa amevunja sheria ya Mose, na hivyo atastahili kuuawa. Ragueli anajua kwamba wewe ndiwe peke yako uliye na haki ya kumwoa binti yake na kupata urithi. Kwa hiyo fuata shauri langu. Nitazungumza na Ragueli usiku huu na kupanga mambo ya uchumba wako na Sara. Tutakaporudi nyumbani kutoka Rage tutamchukua Sara.”
13 Kisha Tobia akamwambia Rafaeli, “Ndugu yangu Azaria, nimekwisha sikia yaliyowapata waume saba wa Sara, jinsi kila mmoja wao alivyokufa ghafla siku ya harusi; kila mmoja alikufa kabla ya kulala naye.
14 Tena nimesikia kwamba jini ndilo lililowaua. Jini hilo halimdhuru Sara, lakini humuua kila mwanamume anayejaribu kumsogelea Sara. Naliogopa jini hilo. Mimi ni mtoto wa pekee kwa wazazi wangu, na kama nikifa wazazi wangu wataaga dunia kwa uchungu wa kifo changu. Hawana hata mwana mwingine wa kuwazika.”
15 Malaika akamjibu, “Hivi umekwisha sahau maagizo ya baba yako? Alikuambia umwoe mwanamke wa kabila lako. Basi, nisikilize kwa makini. Usihangaike juu ya hilo jini. Mchukue Sara! Najua kwamba leo usiku Ragueli atakuruhusu umwoe Sara.
16 Utakapoingia chumbani kulala, chukua ule moyo wa samaki na ini, weka juu ya ubani unaoungua,
17 kusudi moshi wake uenee chumba kizima. Lile jini litakaponusa harufu yake litatimka mbio, na wala halitamsogelea tena Sara.
18 Lakini kabla hamjalala pamoja, lazima msimame na kumwomba Mungu mwenye huruma awaokoe na kuwaoneeni huruma. Usiogope. Tangu mwanzo wa ulimwengu Sara alikuwa ameteuliwa awe mke wako. Utamwokoa kinywani mwa jini, naye atafuatana nawe mpaka nyumbani kwako. Wewe na Sara mtapata watoto wengi ambao mtawapenda sana. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi!” Basi, Tobia aliposikia maneno ya Rafaeli na kutambua kuwa Sara alikuwa jamaa yake kwa upande wa baba, alianza kumpenda Sara na kutamani sana kumwoa.

Generic placeholder image