10

Yudithi aenda kambini mwa Holoferne
1 Yudithi alipomaliza kumlilia Mungu wa Israeli,
2 aliinuka, akamwita mjakazi wake, akashuka na kuingia katika vyumba alivyozoea kutumia wakati wa siku za Sabato na sikukuu.
3 Akalivua vazi lake la gunia na lile la ujane wake, akaoga na kujipaka marashi ya bei kubwa. Akazichana nywele zake, akazifunga kwa utaji na kuvaa mavazi ya fahari aliyokuwa akivaa nyakati za furaha wakati wa uhai wa Manase, mumewe.
4 Akavaa miguuni mwake viatu vyake na kujiremba kwa vito vya thamani: Hazama na vipuli, bangili na vikuku. Alijiremba kiasi cha kumvutia kila mwanamume ambaye angekutana naye.
5 Yudithi akampa mjakazi wake kiriba cha divai na chupa ya mafuta. Mfuko mwingine akaujaza bisi ya shayiri, mikate ya tini kavu, na mikate mingine iliyookwa kulingana na sheria za Kiyahudi. Vitu hivyo vyote kwa pamoja akavifunga kwa uangalifu mkubwa akampa mjakazi wake.
6 Kisha, hao wanawake wawili wakatoka nyumbani, wakaenda kwenye lango la mji wa Bethulia, ambako walimkuta Uzia pamoja na maofisa wa mji: Kabrisi na Karmisi, wakiulinda mji.
7 Wanaume hao walipomwona Yudithi uso wake ukiwa umebadilika na mavazi yake pia walistaajabia uzuri wake wakamwambia,
8 “Mungu wa wazee wetu na akujalie na kuifanikisha mipango yako kwa utukufu wa watu wa Israeli na wa Yerusalemu.”
9 Yudithi akamwomba Mungu; halafu akawaambia, “Waambieni watu wanifungulie lango la mji. Nimo njiani kuutekeleza mpango tuliozungumzia.” Basi wakawaagiza vijana wamfungulie Yudithi lango, kama alivyotaka.
10 Yudithi na mjakazi wake wakatoka mjini. Wale wanaume wakawa wanamwangalia Yudithi akiteremka mlimani hadi bondeni, mpaka waliposhindwa kumwona.
11 Hao wanawake wawili walipokuwa wanatembea bondeni, kikosi cha ulinzi cha Waashuru kikakutana nao.
12 Wakamkamata Yudithi na kumhoji, “Wewe ni wa taifa gani? Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Yudithi akawajibu, “Mimi ni Mwebrania na ninawakimbia Waisraeli kwa sababu Mungu amewatia mikononi mwenu ili kuwaangamiza.
13 Mimi nimo njiani kwenda kumwona Holoferne, jemadari wa jeshi lenu, ili kumpasha habari za kuaminika. Ninaweza kumjulisha namna ya kwenda milimani na kulishika eneo zima bila ya kuwapo majeruhi yoyote katika jeshi lake, wala kutekwa”.
14 Wale wanaume walishangaa kwa uzuri wa Yudithi kwani alikuwa mzuri sana. Walipomsikiliza, wakamwambia,
15 “Umeyaokoa maisha yako kwa kuja hapa kumwona jemadari bwana wetu. Baadhi ya watu wetu watakusindikiza hadi kwenye hema lake na kukutambulisha kwake.
16 Utakapokuwa mbele yake usiwe na hofu yoyote moyoni mwako. Wewe mwambie yale uliyotuambia sisi, naye atakutendea mema.”
17 Hivyo, wakawaagiza watu 100 wamsindikize Yudithi pamoja na mjakazi wake kwenda katika hema la Holoferne.
18 Kwenye kambi yote kulikuwa na msisimko mkubwa kutokana na habari za kufika kwa Yudithi ambazo zilienea kutoka hema hadi hema. Yudithi alipokuwa anasimama nje ya hema ya Holoferne akingojea kuruhusiwa kuingia baada ya Holoferne kuambiwa habari zake, wanajeshi wengi wa jeshi la Waashuru walikuja na kumzunguka Yudithi.
19 Wanajeshi hao walishikwa na bumbuazi kutokana na uzuri wa Yudithi, wakishangaa Waisraeli ni watu wa aina gani! Wakabaki kuulizana wao kwa wao, “Je, nani awezaye kuwadharau watu hawa wenye wanawake kama huyu? Inatupasa kuwaua wanaume Waisraeli wote; la sivyo, watu hawa wataupotosha ulimwengu wote!”
20 Kisha, walinzi wa Holoferne pamoja na watumishi wake binafsi wakatoka nje na kumpeleka Yudithi ndani ya hema.
21 Holoferne, wakati huo, alikuwa akijipumzisha kwenye kitanda chake kilichokuwa kimefunikwa kwa chandarua kilichofumwa kwa nyuzi za zambarau, dhahabu, zumaridi na mawe ya thamani.
22 Walipomweleza kuwa Yudithi amewasili, Holoferne alikuja barazani mwa hema. Taa zilizotiwa nakshi kwa fedha zilichukuliwa mbele ya Holoferne.
23 Yudithi alipofika mbele ya Holoferne na watumishi wake, wote walishikwa na bumbuazi kwa uzuri wa Yudithi. Yudithi aliinama kifudifudi mbele ya Holoferne, lakini watumishi wa Holoferne walimwinua!

Generic placeholder image