12

Yudithi anabaki mwaminifu
1 Holoferne akawaamuru watu wampeleke Yudithi kwenye meza ambako sahani zake za fedha ziliwekwa, na akaandaliwe chakula kutokana na vyakula maalumu anavyokula na kupewa divai.
2 Lakini Yudithi akakataa, akisema, “Siwezi kula chakula hiki, kwani nitakuwa navunja sheria za Mungu wangu. Nitakula tu chakula nilichojichukulia.”
3 Holoferne akamwuliza, “Lakini tutafanya nini wakati chakula chako na divai yako vimekwisha? Tutapata wapi chakula kwa ajili yako? Kambini mwetu hakuna Waisraeli.”
4 Yudithi akamjibu, “Bwana, kwa hakika, kama uishivyo, nina chakula cha kutosha mpaka hapo Mungu atakapokuwa amenitumia kutekeleza mpango wake.”
5 Watumishi binafsi wa Holoferne wakampeleka Yudithi kwenye hema. Akalala huko mpaka asubuhi na mapema alipoamka
6 na kutuma ujumbe kwa Holoferne kuomba ruhusa aende bondeni kuomba.
7 Holoferne akaagiza walinzi wake wamruhusu Yudithi kutoka kambini. Yudithi akakaa kambini kwa muda wa siku tatu, na kila usiku akatoka kwenda bondeni karibu na mji wa Bethulia na kuoga kwenye chemchemi.
8 Baada ya kuoga, alimwomba Bwana Mungu amlinde katika mpango wake wa kuwaletea Waisraeli ushindi.
9 Kisha baada ya kujiweka safi kidini alirudi na kukaa hemani mwake mpaka chakula chake cha jioni kilipoletwa kwake.

Karamu ya Holoferne
10 Siku ya nne ya Yudithi kukaa kambini, Holoferne aliwafanyia karamu maofisa wenye vyeo vya juu, lakini hakuwaita maofisa waliokuwa kwenye zamu ya ulinzi.
11 Alimwambia Bagoa, towashi aliyesimamia mambo yake binafsi, “Nenda ukamshawishi yule mwanamke Mwebrania aliye chini ya ulinzi wako, aje hemani kula na kunywa pamoja nasi.
12 Itakuwa aibu kwetu kumwacha mwanamke mzuri kama yule bila kuzungumza naye. Tusipomkaribisha atatucheka.”
13 Hivyo, Bagoa akamwacha Holoferne, akamwendea Yudithi na kumwambia, “Ee mwanamke mzuri! Jemadari anakualika hemani mwake ili kunywa divai pamoja nasi! Hivyo karibu ufurahie divai pamoja nasi kama mmoja wa wanawake Waashuru wanaohudumu kwenye ikulu ya Nebukadneza. Hii ni heshima kubwa sana kwako”.
14 Yudithi akamwambia, “Mimi ni nani kumkatalia bwana wangu? Nitafanya mara lolote analotaka, nalo litakuwa la kujivunia mpaka siku ya kufa kwangu.”
15 Hivyo, Yudithi akainuka, akavalia mavazi na mapambo yake ya urembo. Mjakazi wake akamtangulia na kuweka mbele ya Holoferne ngozi za mbuzi alizopewa Yudithi na Bagoa ili kukalia anapokula.
16 Yudithi akaingia hemani, akaketi. Holoferne alipomwona Yudithi, moyo ulimdunda kwa shauku kubwa ya kulala naye. (Tangu siku ile ya kwanza, alipomwona Yudithi, Holoferne alikuwa akitafuta nafasi ya kumtongoza.)
17 Holoferne akamwambia Yudithi, “Kunywa, ufurahi pamoja nasi.”
18 Yudithi akamjibu, “Bwana wangu, leo nitakunywa kwani leo ni siku ya maana sana maishani mwangu.”
19 Halafu, mbele yake, alikula na kunywa kile kilichoandaliwa na mjakazi wake.
20 Holoferne alitekwa na uzuri wa Yudithi, akanywa divai nyingi zaidi ya vile alivyowahi kunywa tangu kuzaliwa kwake.

Generic placeholder image