1

Vita kati ya Nebukadneza na Arfaksadi
1 Mfalme Nebukadneza alikuwa mfalme wa Waashuru. Makao yake makuu yalikuwa katika mji mashuhuri wa Ninewi. Wakati huo huo, mfalme Arfaksadi alikuwa akitawala Wamedi. Makao yake makuu yalikuwa mjini Ekbatana.
2 Mfalme Arfaksadi aliuzungushia mji wa Ekbatana ukuta wa mawe. Kimo cha ukuta huo kilikuwa mita 30, na unene wake mita 22. Kila jiwe lilikuwa na unene wa sentimita 130, na urefu wa sentimita 260.
3 Katika kila lango la mji, alijenga mnara wenye kimo cha mita 44, na msingi wenye unene wa mita 26.
4 Kila lango alilijenga liwe na kimo cha mita 30, na upana wa mita 18, ili wanajeshi wake wapite kwa urahisi, wakiwa katika vikosi vyao.
5 Mnamo mwaka wa kumi na mbili wa utawala wake, mfalme Nebukadneza alianzisha vita dhidi ya mfalme Arfaksadi. Vita hivyo vilikuwa kwenye mbuga kubwa ya mji wa Rage.
6 Mataifa mengi yalijiunga na mfalme Arfaksadi. Watu waliojiunga naye ni: Watu wote waliokuwa wanakaa milimani, waliokaa kandokando ya mito ya Tigri, Eufrate na Hidaspe. Pia walijiunga naye watu waliokaa kwenye mbuga iliyotawaliwa na mfalme Arioko wa Elamu. Mataifa mengi yalijiunga katika ushirika ulioitwa Jumuiya ya Kelodi.
7 Kisha, Nebukadneza, mfalme wa Waashuru, aliwapelekea ujumbe Wapersi na watu wa magharibi, katika maeneo ya Kilikia, Damasko, Lebanoni, Antilebanoni na watu wote waliokaa pwani
8 na watu waliokaa huko Karmeli, Gileadi, Galilaya ya kaskazini, pamoja na watu waliokaa kwenye tambarare ya Yezreeli.
9 Mfalme Nebukadneza aliwapelekea pia ujumbe watu waliokaa huko Samaria na miji ya jirani, wale waliokaa magharibi ya mto Yordani mpaka miji ya Yerusalemu, Bethania, Kelusi, Kadeshi na wilaya ya Gosheni. Ujumbe huo pia walipelekewa watu waliokaa katika miji ya Misri, yaani Tahpanesi, Ramesesi, na eneo lote la Gosheni.
10 Ujumbe huo ulipelekwa hadi miji ya Tanisi na Memfisi, na hadi kwenye mpaka wa Misri na Ethiopia.
11 Lakini watu wote wa eneo hilo walipuuza ujumbe wa mfalme Nebukadneza, mfalme wa Waashuru. Walikataa kuungana naye vitani kwani hawakumwogopa. Waliona kuwa hakukuwa na uwezekano wa yeye kushinda vita hivyo. Wakawarudisha wajumbe wake wakiwadharau na kuwaacha waende mikono mitupu.
12 Mfalme Nebukadneza alilikasirikia sana eneo lote. Akaapa kutumia utajiri wote wa ufalme wake katika kuwalipiza kisasi watu wa eneo hilo waliokataa kujiunga naye. Aliapa kuwa ataiangamiza jumuiya nzima iliyokaa huko Kilikia, Damasko, Ashuru, Moabu, Amoni, Yudea, na Misri. Aliapa pia kuwaua watu wote waliokaa pwani ya bahari ya Mediteranea hadi Persia.
13 Mnamo mwaka wa kumi na saba wa utawala wake, mfalme Nebukadneza aliyaongoza majeshi yake kumshambulia mfalme Arfaksadi, akamshinda. Nebukadneza akayashinda majeshi ya Arfaksadi, kikosi cha wapandafarasi pamoja na kikosi cha magari ya vita.
14 Hivyo, mfalme Nebukadneza akaimiliki miji yote kwenye nchi ya Umedi. Akasonga mbele ili kuushambulia mji wa Ekbatana. Akaiteka minara ya mji, masoko na uzuri wa mji huo akaufanya magofu.
15 Akamteka mfalme Arfaksadi kwenye milima iliyoko kandokando ya mji wa Ragau na kumuua kwa mikuki ya kuwindia.
16 Baada ya kumuua mfalme Arfaksadi, mfalme Nebukadneza, pamoja na majeshi yake yote, alirudi mjini Ninewi akiwa na mali nyingi sana alizoteka nyara vitani. Akiwa huko Ninewi, yeye pamoja na wanajeshi wake, walipumzika na kufanya sherehe kwa muda wa miezi minne.

Generic placeholder image