3

Ujumbe wa amani kwa mfalme Nebukadneza
1 Watu wote wa eneo lote la magharibi wakampelekea mfalme Nebukadneza ujumbe wa amani, wakisema,
2 “Sisi tunabaki kuwa watiifu kwako mfalme mkuu Nebukadneza. Tumo mikononi mwako na tu tayari kukutii na kukutumikia jinsi upendavyo.
3 Majengo yetu, nchi yetu yote, mashamba yetu ya ngano, mifugo wetu na mahema yetu vipo chini ya mamlaka yako; vitumie upendavyo.
4 Watu wetu ni watumwa wako, na unaweza kuitumia miji yetu upendavyo.”
5 Baada ya wajumbe wa amani kuleta ujumbe wenyewe,
6 Holoferne aliliongoza jeshi hadi pwani ya bahari ya Mediteranea. Akaweka ulinzi kwenye miji yote iliyozungushiwa kuta na kuchagua wanaume wenyeji kuwa jeshi la akiba.
7 Watu wote pamoja na wale wa nchi jirani walimkaribisha Holoferne kwa ngoma huku wamevaa taji za maua.
8 Lakini Holoferne alipabomolea mbali mahali pao pote pa ibada na kukatilia mbali miti yao mitakatifu. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa ameagizwa kuvunjilia mbali sanamu zote za miungu ili mataifa yamwabudu Nebukadneza peke yake, na kwamba watu wa kila lugha na taifa wamwite mungu wao.
9 Kisha, Holoferne akapita katikati ya Bonde la Yezreeli karibu na Dothani, mkabala na milima ya Yuda.
10 Akapiga kambi kati ya miji ya Geba na Sithopoli. Akakaa huko ili kukusanya vifaa vya jeshi lake.

Generic placeholder image