9

Sala ya Yudithi
1 Yudithi alianguka kifudifudi akajipaka majivu kichwani, akalifunua vazi lililofunika vazi la ndani la gunia; wakati huo huo watu walikuwa wanafukiza ubani hekaluni wakati wa jioni, mjini Yerusalemu. Ndipo Yudithi alipomlilia Bwana kwa sauti kubwa akisema,
2 “Ee Bwana, Mungu wa Simeoni babu yangu, kumbuka jinsi ulivyomtia nguvu babu yangu Simeoni kuwalipiza kisasi kwa upanga wale wageni waliomshika msichana Dina kwa nguvu, wakamvua nguo zake na kumwaibisha, wakamnajisi huyo aliyekuwa bikira na kumfedhehesha.
3 Ndiyo maana uliwatoa viongozi wao wauawe kwenye kile kitanda walimomshikia kwa nguvu Dina. Uliwaangamiza watumwa, pamoja na hao wakuu pamoja na wafuasi wao.
4 Uliwaacha wake zao wachukuliwe, binti zao wachukuliwe mateka na nyara zao zigawanywe miongoni mwa hao uliowapenda yaani Waisraeli ambao walikuwa tayari kufanya matakwa yako. Kaka za Dina walikasirika kutokana na kuaibishwa kwa dada yao. Hivyo walipokuomba kuwasaidia uliwapa msaada. “Ee Mungu, Mungu wangu, nisikilize nami niliye mjane;
5 kwani umefanya yaliyopita, yanayotukia sasa na yatakayofuata baadaye. Yaliyopo yatakayokuwapo, wewe ndiwe umeyapanga; mambo ambayo uliyaazimia yametendeka.
6 Makusudi yako yamefanyika nayo husema, ‘Tazama tuko hapa!’ Maana mipango yako yote hutekelezwa; wajua utakavyoamua hata kabla.
7 “Sasa Bwana, Waashuru wana nguvu kuliko awali, na kiburi chao hutokana na wanajeshi wao wa miguu na wapandafarasi. Wao wanategemea silaha zao, lakini hawajui kuwa, wewe ee Bwana, ndiwe shujaa ukomeshaye vita. Bwana ndilo jina lako.
8 Kwa hasira yako, tumia nguvu zako kulivunja jeshi lao lenye nguvu. Wanapanga kulitia unajisi hekalu lako ambamo unaabudiwa. Pia wanapanga kuzibomoa pembe za madhabahu yako kwa mapanga yao.
9 Ona walivyo na kiburi! Uwamwagie ghadhabu yako! Mimi ni mjane, lakini nakuomba unipe nguvu ili nitekeleze mpango wangu.
10 Nakuomba utumie maneno yangu yenye hila kuwaangamiza wote, bwana na mtumwa. Naam, mkono wa mwanamke na uvunjilie mbali kiburi chao.
11 Nguvu yako haitegemei wingi wa wanajeshi wala uwezo wao. Wewe ni Mungu wa wanyenyekevu na unawasaidia wanaokandamizwa. Walio wanyonge na wasio na msaada unawapa msaada. Waliokata tamaa unawaokoa.
12 Ee Mungu wa babu yangu Simeoni, wewe unayetumainiwa na Waisraeli, Bwana wa mbingu na dunia, Muumba wa maji, na Mfalme wa viumbe vyote, nakuomba uisikilize sala yangu.
13 Nakuomba uyafanye maneno yangu ya hila yadhuru na kuua wale waliopanga mabaya dhidi ya agano lako na hekalu lako, dhidi ya mlima wako Siyoni na nchi yote uliyowapa watu wako.
14 Lifanye taifa lako lote na kila kabila lijue kuwa wewe ndiwe Mungu mwenye nguvu na uwezo wote, na kuwa ni wewe peke yako unayewalinda Waisraeli.”

Generic placeholder image