11

1 Holoferne akamwambia Yudithi, “Jipe moyo mama! Hakuna haja kwako kuwa na hofu moyoni mwako! Sijamdhuru yeyote anayechagua kumtumikia Nebukadneza, mfalme wa dunia nzima.
2 Hata sasa, watu wako wanaokaa milimani wangekuwa hawajanitusi, nisingetangaza vita dhidi yao. Walijiletea taabu hii yote wao wenyewe.
3 Lakini, niambie, kwa nini umetoroka na kukimbilia kwetu? Utakuwa salama kabisa. Usiwe na wasiwasi; utaishi usiku huu na siku zijazo.
4 Hakuna mtu yeyote atakayekudhuru; bali kila mmoja atakutendea kwa wema kama watumishi wengine wa bwana wangu, mfalme Nebukadneza.”
5 Yudithi akamwambia Holoferne, “Nakuomba uniruhusu nizungumze nawe, bwana, na nakuomba uyategee masikio maneno yangu mimi mjakazi wako ninayotaka kusema mbele yako. Nitakuambia kweli tupu.
6 Ikiwa utafuata mashauri yangu, mimi mjakazi wako, Mungu atafanya makubwa kwa njia yako, nawe kwa hakika mipango yako itafaulu.
7 Ninaapa kwa maisha na uwezo wa Nebukadneza, mfalme wa dunia nzima, aliyekutuma kuleta utengemano kati ya raia wa ufalme wake, kuwa si tu kwamba umewafanya watu wote wamtumikie yeye, bali kutokana nawe hata wanyama wa porini, mifugo na ndege, vyote vinamtii yeye. Kutokana nawe Nebukadneza atastawi na ufalme wake wote.
8 Tumesikia hekima yako na werevu wako. Dunia nzima inajua kuwa wewe ni mtu mwema, mwenye maarifa na mwenye ujuzi mkubwa kuhusu mambo ya vita.
9 Akioro aliyeokolewa na watu wetu ametusimulia yale aliyosema kwenye kikao chako cha halmashauri.
10 Kwa hiyo ee bwana, yale aliyosema usiyatupilie mbali kana kwamba ni upuuzi mtupu, nakuomba myatie maanani sana, kwani aliyosema ni ukweli mtupu. Hakuna mtu yeyote anayeweza kulidhuru taifa letu, sembuse kulishinda, isipokuwa liwe limetenda dhambi dhidi ya Mungu wake.
11 “Lakini hutapata hasara yoyote wala hutashindwa kutekeleza lengo lako. Wakati Waisraeli wanatenda dhambi na hivyo kumkasirisha Mungu wao, kwa hakika watakufa.
12 Sasa hivi, akiba ya chakula chao imewaishia, na maji yao yote karibu yamewaishia. Na kwa sasa hivi, wameamua kuchinja mifugo yao na kula vyakula ambavyo sheria ya Mungu wao inawakataza.
13 Wameamua kula malimbuko ya mavuno ya ngano, zaka za divai na mafuta, vitu ambavyo ni vitakatifu, navyo hutumiwa na makuhani tu wanaomhudumia Mungu mjini Yerusalemu. Sisi watu wengine haturuhusiwi hata kuvigusa vyakula hivi vitakatifu.
14 Lakini kwa kuwa watu mjini Yerusalemu wamekwisha vunja sheria hiyo, watu wa mji wetu, wamepeleka watu mjini Yerusalemu kuomba idhini ya kufanya kama wao kutoka halmashauri kuu.
15 Siku hiyo ambayo watapatiwa kibali hicho na kula chakula hicho, utaweza kuwaangamiza.
16 Mara moja nilipojua hayo, niliwatoroka watu wangu. Na Mungu amenituma kufanya kitu fulani pamoja nawe ambacho kitawashangaza watu katika dunia nzima watakaposikia juu yake.
17 “Mimi ni mwanamke mcha Mungu sana. Ninamwabudu Mungu wa mbinguni mchana na usiku. Nitabaki kambini mwako, lakini kila siku usiku nitakwenda bondeni kumwomba Mungu, naye atanijulisha wakati Waisraeli watakapotenda dhambi.
18 Mara moja nitakapojua jambo hilo, nitakuja na kukujulisha, ndipo utakapotoka na jeshi lako lote. Na hakuna Mwisraeli yeyote atakayeweza kukupinga.
19 Nitakuongoza kupitia katikati ya nchi ya Yuda hadi mjini Yerusalemu, huko nitakutawaza kuwa mfalme katikati ya mji huo. Halafu utaweza kuwatawanya wakazi wa mjini Yerusalemu kama kondoo wasio na mchungaji. Hata mbwa hatathubutu kukubwekea. Mungu amenifunulia mambo haya mapema, naye amenituma kukujulisha.”
20 Holoferne pamoja na watumishi wake binafsi walifurahishwa sana na habari hizo za Yudithi, wakashangaa jinsi alivyo na hekima.
21 Wakasema wao kwa wao, “Yamkini hakuna mwanamke kama yeye duniani kote aliye mzuri kwa umbo na mwenye kusema kwa hekima.”
22 Kisha, Holoferne akamwambia Yudithi, “Ni jambo jema sana kuwa Mungu amekutuma kuwatangulia wengine, ili kututia nguvu, nao waliomtukana bwana wangu wapate kuangamizwa.
23 Wewe ni mzuri kwa umbo na unasema kwa hekima. Ukifanya kama ulivyoahidi, basi, Mungu wako atakuwa ndiye Mungu wangu. Utaishi katika ikulu ya Nebukadneza na utakuwa mwanamke maarufu katika dunia nzima.”

Generic placeholder image