5

Halmashauri ya vita kambini mwa Holoferne
1 Holoferne, jenerali wa jeshi la Ashuru, aliposikia kuwa watu wa Israeli wamejitayarisha kwa vita kwa kufunga njia za milimani, wamejenga ngome milimani, na kuweka vizuizi vya barabarani mbugani,
2 aliwaka hasira. Hivyo, aliwaita wakuu wa Wamoabu, makamanda wa Waamoni na magavana wote wa eneo la pwani ya bahari ya Mediteranea.
3 Walipokusanyika, aliwaambia, “Nyinyi mnaokaa katika nchi hii ya Kanaani, hebu niambieni, ni watu wa namna gani wanaokaa katika milima hii? Wanakaa katika miji gani? Je, jeshi lao ni kubwa kiasi gani? Je, uwezo na nguvu zao vinatokana na nini? Je, ni nani mfalme anayelitawala na kuliongoza jeshi lao?
4 Kwa nini wamekataa kujitokeza ili kunilaki kama watu wengine wa magharibi?”

Hotuba ya Akioro
5 Ndipo Akioro, kiongozi wa Waamoni wote, alipomwambia Holoferne, “Bwana, nakuomba mimi mtumishi wako, usikilize ninalotaka kusema. Nitakueleza ukweli kuhusu watu wanaokaa kwenye milima karibu na wewe. Mimi mtumishi wako sitakuambia uongo wowote.
6 Watu hao ni wazawa wa Wakaldayo.
7 Hapo zamani walikaa katika nchi ya Mesopotamia. Lakini kwa sababu hawakuweza kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao huko Ukaldayo,
8 wala hawakuzifuata njia zao, wakahama ili kumwabudu Mungu wa mbinguni. Mungu waliyejifunza kumkiri. Walipofukuzwa toka mbele ya miungu yao wenyewe, walikimbilia Mesopotamia, ambako walikaa kwa muda mrefu.
9 “Baada ya muda fulani, Mungu wao aliwaamuru waiache nchi ya Mesopotamia, waende kukaa katika nchi ya Kanaani. Huko wakastawi sana wakiwa na dhahabu nyingi, fedha na mifugo mingi.
10 Njaa ilipotokea katika nchi nzima ya Kanaani, walisafiri mpaka Misri ambako walikaa wakapata chakula cha kutosha. Wakiwa huko wakawa kundi kubwa la watu - wengi hata hawakuweza kuhesabika.
11 Hivyo, mfalme wa nchi ya Misri, akaanza kuwa na uhasama dhidi yao. Aliwatumia kufyatua matofali. Alishusha hadhi yao na kuwafanya watumwa.
12 Lakini wakamlilia Mungu wao; naye akaipiga nchi ya Misri kwa kuiletea maafa yasiyoponyeka. Basi Wamisri wakawafukuza nje ya nchi yao.
13 Walipofika kwenye Bahari ya Shamu, Mungu wao akaikausha hiyo bahari mbele yao,
14 akawaongoza hadi kwenye mlima Sinai na Kadesh-barnea. Baada ya kuwafukuzia mbali wakazi wa jangwani;
15 walifanya makao yao katika nchi ya Waamori, na kwa kutumia nguvu zao waliwaulia mbali wakazi wa Heshboni. Halafu walipovuka mto Yordani walimiliki eneo lote la milimani.
16 Kisha baada ya kuwafukuza Wakanaani, Waperizi, Wayebusi, Washekemu na Wagirgashi, walikaa katika eneo hilo kwa muda mrefu.
17 Wakati wote ambao hawakutenda dhambi, walistawi, maana Mungu wao ni Mungu anayechukia uovu.
18 Lakini walipoiacha njia aliyowaagiza waifuate walishindwa katika vita vingi na kupelekwa mateka hadi nchi nyingine. Hekalu la Mungu wao lilibomolewa na miji yao ilikaliwa na maadui zao.
19 Basi baada ya kumrudia tena Mungu wao kwanza walirudi kutoka nchi walikohamishiwa na kutawanywa. Wameushika mji wa Yerusalemu ambao kuna hekalu lao na wanaimiliki tena milima ambayo haikukaliwa na mtu.
20 “Sasa bwana mkubwa, ikiwa watu hawa wamefanya kosa lolote, kama wametenda dhambi dhidi ya Mungu wao, kwanza inatupasa tuwe na uhakika kwamba ni kweli wana sababu ya kushindwa vitani, halafu tuwashambulie.
21 Lakini ikiwa hawajavunja sheria yoyote, basi, na tuwaache watu hawa, tukiogopa kwamba Mungu wao atawatetea, la sivyo, sisi tutaaibika duniani kote.”

Hoja za watu
22 Mara tu Akioro alipomaliza hotuba yake, watu walisimama na kuanza kupinga. Maofisa wakuu wa Holoferne, Wamoabu pamoja na watu wote kutoka pwani ya bahari ya Mediteranea walitaka Akioro auawe.
23 Wakauliza, “Kwa nini tuwaogope Waisraeli, watu ambao hawana nguvu wala uwezo wa kupigana?
24 Songa mbele! Endelea! Ee mkuu wetu Holoferne, jeshi lako litawameza mara moja.”

Generic placeholder image