14

Mpango wa Yudithi
1 Ndipo Yudithi akawaambia, “Ndugu zangu, nisikilizeni sasa, kichukueni kichwa hiki na kukitundika kwenye ukuta wa mji.
2 Chagueni kiongozi, na asubuhi na mapema jua linapochomoza, wachukueni wanaume mashujaa wakiwa na silaha zao, watoke nje ya mji, kana kwamba wanakwenda bondeni kukishambulia kituo cha Waashuru; lakini msishuke.
3 Walinzi wa Waashuru watachukua silaha zao na kukimbilia kambini ili kuwaamsha maofisa wao. Maofisa watakimbia kwenye hema la Holoferne kumwamsha, lakini hawatamkuta. Hapo jeshi lote litaduwaa na kurudi nyuma huku nyinyi mnasonga mbele kuwashambulia.
4 Ndipo nyinyi pamoja na Waisraeli wote mtaweza kuwafuatia na kuwaua wanapokimbia.
5 Lakini kabla hamjafanya yote haya, nileteeni Akioro, Mwamoni, ili amuone na kumtambua yule mtu aliyewadharau watu wa Israeli, na aliyempeleka Akioro kwetu, akifikiri kuwa Akioro angeuawa.”

Akioro anakuwa Mwisraeli
6 Hivyo, wakamwita Akioro kutoka nyumbani kwa Uzia. Lakini alipokuja na kukiona kichwa cha Holoferne mikononi mwa mtu mmoja katika mkutano wa watu alianguka chini na kuzimia.
7 Walipomsaidia kusimama wima, Akioro aliinama mbele ya Yudithi mpaka chini, akasema, “Umebarikiwa wewe katika kila jamaa ya Yuda; na katika kila taifa wale watakaosikia jina lako watashikwa na hofu.
8 Sasa tafadhali, nieleze yote uliyoyatenda katika siku hizi zilizopita.” Watu wote wa mji walipokusanyika, Yudithi akaeleza yote, jinsi alivyofanya tangu siku alipoondoka mjini mpaka wakati huo.
9 Baada ya kumaliza kuwaeleza, watu walipiga vigelegele vya furaha na mji mzima ukawaitikia.
10 Akioro aliposikia yote aliyotenda Mungu wa Israeli, alimwamini Mungu kwa dhati. Akioro akatahiriwa na kufanywa mmoja wa jumuiya ya Kiisraeli, na ndivyo walivyo wazawa wake mpaka leo.

Hofu kambini kwa Holoferne
11 Kesho yake asubuhi, Waisraeli wakakitundika kichwa cha Holoferne kwenye ukuta wa mji. Wanaume wote wakatwaa silaha zao na kutoka wakiwa kwenye vikosi vyao. Wakaanza kuiteremka miteremko ya mji.
12 Mara Waashuru walipowaona, wakapeleka taarifa kwa wakuu wao, nao wakuu wakawapelekea majenerali wao, makamanda wao wa maelfu na maofisa wengine.
13 Hao wakuu wakaenda kwenye hema la Holoferne na kumwambia aliyesimamia shughuli za binafsi za Holoferne, “Mwamshe jemadari! Wale watumwa Waisraeli wamethubutu kushuka huku kutoka mlimani ili kupigana nasi ili waangamie!”
14 Bagoa akaingia ndani ya hema na kutikisa pazia ya chumba cha kulala hemani (kwani alidhani Holoferne alikuwa kitandani na Yudithi).
15 Lakini alipoona hakuna jibu, alilivuta kwa upande hilo pazia na kuingia ndani. Kutahamaki, akaukuta mwili wa Holoferne bila kichwa kwenye kiti kidogo cha miguu.
16 Bagoa akapiga yowe, akatoa kilio cha huzuni, akaomboleza, akapiga kelele na kurarua mavazi yake.
17 Akaenda ndani ya hema alimokuwa analala Yudithi, alipoona hayumo alikimbia nje na kuwaita maofisa kwa sauti kubwa,
18 “Wale watumwa wametulaghai! Mwanamke mmoja tu Mwisraeli ameuletea aibu ufalme mzima wa Nebukadneza. Tazameni! Holoferne yuko chini, amebaki kiwiliwili tu bila kichwa!”
19 Maofisa waliposikia habari hizo, waliyararua mavazi yao kwa huzuni; vilio na makelele yao vilisikika katika kambi nzima.

Generic placeholder image