13

1 Mwishowe, usiku ulipoingia, wageni wakaomba radhi kuondoka; wakaenda zao. Kisha Bagoa akalifunga hema kwa nje na akawazuia watumishi wa Holoferne kuingia ndani. Hivyo wote wakaenda kulala; kila mmoja alikuwa amechoka kwa sababu karamu ilichukua muda mrefu mno.
2 Yudithi akabaki peke yake hemani pamoja na Holoferne ambaye alikuwa amejitupa kitandani kwa sababu alikuwa amelewa sana.
3 Yule mjakazi wa Yudithi akawa anamngojea Yudithi nje ya chumba cha kulala hemani anapotoka kwenda kuomba, kama alivyofanya kila usiku. Yudithi pia alikuwa amemwambia Bagoa kuwa angetoka usiku kwenda kuomba, kama ilivyokuwa kawaida yake.
4 Wakati huo, wageni wote mashuhuri na watu wa kawaida walikuwa wamekwisha kwenda zao, wakabaki Yudithi na Holoferne peke yao chumbani. Yudithi akasimama kandoni mwa kitanda cha Holoferne, akaomba kimyakimya, “Ee Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, nisaidie katika tendo hili ninalotaka kutenda kwa ajili ya utukufu wa mji wa Yerusalemu.
5 Sasa ndio wakati wa kuwaokoa watu wako wateule; unisaidie mimi kutekeleza mpango wangu wa kuwaangamiza maadui walioinuka dhidi yetu.”
6 Yudithi akaenda karibu na tendegu karibu na kichwa cha Holoferne, akaufyatua upanga wa Holoferne ulioninginia hapo.
7 Akasogea karibu kabisa, akazikamata nywele za Holoferne, akasema, “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nipe nguvu sasa!”
8 Kisha Yudithi akainua upanga na kumkata Holoferne mara mbili shingoni kwa nguvu zake zote, akakichopoa kichwa cha Holoferne.
9 Mwili wa Holoferne akausukumia chini ya kitanda na kukivutia chini chandarua. Kisha akatoka nje na kumpa mjakazi wake kichwa cha Holoferne.
10 Mjakazi akakitia kwenye mfuko wa chakula.

Yudithi na mjakazi wake wanarudi Bethulia
Basi, Yudithi na mjakazi wake wakaondoka, kama ilivyokuwa desturi yao, wakaenda kuomba. Walipokwisha toka katika kambi ya Waashuru, walipita bonde na kupanda milimani mpaka wakakaribia malango ya mji wa Bethulia.
11 Walipokuwa mbali kiasi, Yudithi akawaita walinzi waliokuwa langoni, akasema, “Fungueni lango! Fungueni lango! Mungu wetu bado yu pamoja nasi. Leo tena ameonesha uwezo wake katika Israeli, na ametumia nguvu zake dhidi ya maadui zetu.”
12 Wanaume waliposikia sauti ya Yudithi, walipiga mbio kwenda kwenye malango na kuwaita wazee wa mji.
13 Kila mtu, kijana kwa mzee, walikimbia kwenda kwenye malango. Hakuna aliyeweza kusadiki kuwa kweli Yudithi amerudi. Wakamfungulia lango akiwa pamoja na mjakazi wake, wakawakaribisha. Kisha, wakawasha moto ili wapate mwanga, wakawazunguka wale wanawake wawili.
14 Yudithi akapaaza sauti yake, akasema, “Msifuni Mungu! Naam, mpeni yeye sifa. Msifuni Mungu ambaye hajaacha kuwahurumia watu wa Israeli. Leo usiku amenitumia kuwaangamiza maadui zetu.”
15 Kisha alipokitoa kichwa cha Holoferne kwenye mfuko wa chakula na kuwaonesha watu waliokusanyika, akawaambia, “Hiki hapa kichwa cha Holoferne, jemadari wa jeshi la Waashuru. Na hiki hapa chandarua toka kitanda chake alikolala fofofo, akiwa amelewa sana. Bwana amemtumia mwanamke kumuua Holoferne.
16 Naapa kwa jina la Bwana aliyenilinda katika kazi niliyokuwa nayo, hivyo uzuri wangu ukampumbaza Holoferne hata akakifikia kifo chake; Holoferne kamwe hakutenda dhambi nami, hakunitia unajisi wala kuniaibisha.”
17 Kila mmoja mjini alishikwa na bumbuazi. Wakainama chini na kumsujudia Mungu, wakaomba wakisema, “Usifiwe wewe Mungu wetu, uliyewashinda leo maadui za watu wako.”
18 Kisha Uzia akasema, “Yudithi, binti yangu, Mungu Mkuu amekubariki kuliko wanawake wote duniani. Tumsifuje Mungu Bwana Mungu aliyeumba mbingu na dunia! Alikuongoza ulipokuwa unakikata kichwa cha adui yetu mkuu.
19 Imani yako kwa Mungu kamwe haitasahauliwa na wale ambao watasimulia nguvu za Mungu.
20 Mungu na akutunukie heshima ya kudumu kwa yote uliyotenda. Mungu na akupe baraka kwa sababu ulibaki mwaminifu kwake na hukusita kuyahatarisha maisha yako taifa letu lilipodhoofishwa. Ulisonga mbele kupambana na angamizo lililotutisha, ukashika njia iliyonyoka mbele ya Mungu wetu.” Watu wote wakaitikia, “Amina, Amina!”

Generic placeholder image