16

Wimbo wa sifa wa Yudithi
1 Yudithi aliimba: “Msifuni Mungu wangu kwa ngoma, msifuni Bwana wangu kwa matoazi; mwimbieni zaburi na nyimbo za shangwe; mtukuzeni na kumwomba.
2 Maana, Mungu ni Bwana akomeshaye vita. Aliniokoa mikononi mwa walionifuatia, akanirudisha kwenye kambi ya watu wake.
3 “Waashuru walishuka chini kutoka milima ya kaskazini; walishuka na wanajeshi kumi elfu. Wanajeshi wao waliiziba mito mabondeni; na wapandafarasi wao waliijaza milima.
4 Alitishia kuitia moto nchi yangu, kuwaua vijana wangu kwa upanga, kuwabwaga chini wachanga wangu, kuwachukua mateka watoto wangu, na kuwateka nyara wasichana wangu.
5 Lakini Bwana, Mwenyezi-Mungu aliwaangamiza kwa mkono wa mwanamke.
6 Shujaa wao hakuuawa na vijana wala na mashujaa wenye nguvu; wala majitu marefu hayakumvamia. Bali Yudithi binti Merari, ndiye aliyemwangusha kwa uzuri wake.
7 “Akawaletea ushindi Waisraeli waliokandamizwa, alipoondoa mavazi yake ya ujane, akajipodoa usoni mwake kwa marashi.
8 Alisuka nywele zake kwa utaji, akavaa kitani ili kumtega.
9 Kiatu chake kilimfurahisha macho yake, uzuri wake ukaunasa moyo wake. Nao upanga ulikatakata shingo yake.
10 Wapersi walitetemeshwa na uhodari wake; naam, Wamedi walishangazwa na ujasiri wake.
11 “Hao walishikwa na hofu, watu wangu waliodhoofika walipopiga kilio cha vita; hao walishikwa na tisho, watu wangu walio dhaifu walipopiga kelele; hata walikimbia hapo watu wangu walipopaaza sauti.
12 Wana wa watumwa wa kike waliwachoma, waliwajeruhi kama wana wa watoro; waliangamizwa na jeshi la Bwana wangu.
13 “Nitamwimbia wimbo mpya Mungu wangu. Ee Bwana, wewe u mkuu na mtukufu! U mwenye nguvu sana, huwezi kushindwa.
14 Viumbe vyako vyote na vikutumikie wewe! Maana ulisema na vyote vikawapo; ulivipulizia pumzi na vyote vikawa vimeumbwa. Hakuna anayeweza kupinga neno lako.
15 Hata milima na bahari vitatetemeka katika misingi yake kama maji, miamba itayeyuka kama nta mbele yako. Lakini kwa wale wanaokucha wewe bado utawahurumia.
16 tambiko zote za harufu nzuri si kitu kwako; mafuta ya sadaka zote za kuteketezwa ni kitu kidogo kwako.
17 “Ole wao mataifa yanayozusha vita dhidi ya watu wangu. Bwana Mwenye Nguvu atawalipiza kisasi siku ya hukumu. Atatuma moto na mabuu kula miili yao, nao watalia kwa maumivu milele.”

Umaarufu wa Yudithi
18 Watu walipowasili mjini Yerusalemu walimwabudu Mungu, nao baada ya kutakaswa walitoa tambiko zao za kuteketezwa, tambiko za hiari na matoleo yao.
19 Vitu vyote vilivyokuwa vya Holoferne ambavyo watu walimpa Yudithi, na chandarua alichokichukua mwenyewe kutoka kitanda cha Holoferne, Yudithi aliviweka wakfu kwa Mungu kuwa viwe sadaka kwa Bwana.
20 Kwa muda wa miezi mitatu watu waliendelea kufanya sikukuu mbele ya hekalu mjini Yerusalemu. Yudithi akakaa huko pamoja nao.
21 Baada ya sikukuu kumalizika, kila mmoja alirudi nyumbani kwake. Yudithi naye akarudi mjini Bethulia na kukaa kwenye shamba lake. Kwa muda wa maisha yake yote Yudithi alipata heshima katika nchi yote ya Israeli.
22 Wanaume wengi walitaka kumwoa, lakini hakuolewa tena baada ya kifo cha Manase, mumewe.
23 Bali sifa zake zikazidi kuenea. Yule mjakazi wake akampa uhuru. Akaendelea kuishi katika nyumba aliyoiacha Manase, mumewe, hata kupata umri wa miaka 105. Alimpa mjakazi wake uhuru. Kisha Yudithi akafariki. Wakamzika mjini Bethulia kwenye pango la marehemu mumewe.
24 Waisraeli wakamwombolezea kwa muda wa siku saba. Hata hivyo, kabla hajafariki, Yudithi aliwagawia jamaa wa marehemu mumewe mali zake, kadhalika na jamaa zake mwenyewe wa karibu.
25 Hakuna mtu yeyote aliyethubutu kuwatisha Waisraeli wakati wa uhai wa Yudithi, na hata miaka mingi baada ya kifo chake.

Generic placeholder image