7

Mji wa Bethulia unazingirwa
1 Kesho yake, Holoferne akakusanya jeshi lake pamoja na wanajeshi wengine waliojiunga naye. Akaliagiza kwenda kuushambulia mji wa Bethulia, kushika njia zote za mlima na kuwashambulia watu wa Israeli.
2 Wakahamisha kambi yao hadi bondeni karibu na mji wa Bethulia. Jeshi lake lilikuwa kubwa sana, likiwa na wanajeshi wa miguu 170,000, wanajeshi wapandafarasi 12,000 bila kutaja idadi ya vifaa vya kijeshi na wale waliovibeba wakitembea.
3 Kambi yao waliyopiga bondeni karibu na mji wa Bethulia kando ya kijito, ilikuwa kubwa sana, ilienea tangu mji wa Dothani hadi mji wa Balbaimu kwa upana, na kutoka Bethulia hadi mji wa Kyamoni, mkabala na Esdreloni kwa urefu.
4 Waisraeli walipoona ukubwa wa jeshi, waliogopa mno, wakaambiana wao kwa wao, “Wanajeshi hao watakula kila kitu watakachopata. Hata chakula chote kilichoko milimani, mabondeni na vilimani kikiwekwa pamoja, hakiwezi kuwatosha.”
5 Waisraeli wote kwa hofu walichukua silaha zao, wakawasha mienge kwenye minara na kushika ulinzi usiku kucha.
6 Kesho yake, Holoferne aliliongoza jeshi lake la wanajeshi wa miguu ili watu wa Israeli walioko mjini Bethulia waweze kuliona vizuri.
7 Akakagua njia zinazoingia mjini na chemchemi zilizoleta maji mjini. Kabla hajarudi kambini, akaziteka chemchemi na kuweka ulinzi.
8 Viongozi wote wa kijeshi wa Waedomu na Wamoabu, pamoja na makamanda wa pwani ya bahari ya Mediteranea, wakaenda kwa Holoferne, wakamwambia,
9 “Mkuu wetu, tunakuomba usikilize shauri letu ili jeshi lako lisije likashindwa.
10 Hawa watu, Waisraeli, hawategemei ulinzi wao kutokana na silaha, bali kimo cha milima wanakokaa, na si rahisi kukwea milima yao hiyo.
11 Hivyo inafaa kushambulia moja kwa moja ili wanajeshi wako wasiumie au kuuawa.
12 Wewe ubaki kambini ukiwaangalia wanajeshi kwenye hema zao. Jambo la maana ni kuzishika chemchemi zilizoko chini ya milima,
13 maana ndizo zinazowapatia wakazi wa Bethulia maji. Kiu kitawafanya wajisalimishe wenyewe kwako. Wakati huo huo, sisi pamoja na watu wetu tutakwea kwenye vilele vya milima ambako tutapiga kambi na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeutoroka mji.
14 Watadhoofika kwa njaa, pia wanawake wao na watoto wao, hata kabla hatujawashambulia, watakuwa tayari wamelala barabarani nje ya nyumba zao.
15 Kwa njia hiyo, utajilipiza kisasi kwa kuwa walikuasi, wala hawakuja kukulaki kwa amani.”
16 Holoferne pamoja na watu wake walifurahishwa sana na mpango huo. Hivyo akaamua kufanya kama walivyotoa ushauri.
17 Kwa hiyo, wanajeshi Wamoabu pamoja na wanajeshi 5,000 na Waashuru wakahamishia kambi yao bondeni ili kushika chanzo cha maji ya mji.
18 Waedomu na Waamoni wakaenda na kupiga kambi yao kwenye milima mkabala na Dothani. Baadhi ya watu wao wakawapeleka upande wa kusini-mashariki mkabala na mji Egrebeli karibu na mji wa Chusi, kandokando ya mto Mokmuri. Jeshi lote la Waashuru lililobaki lilipiga kambi yao bondeni, likaenea katika nchi nzima. Mahema yao na vifaa vya kijeshi vilifanya kambi iwe kubwa, kwani vilikuwa vingi sana.
19 Basi, Waisraeli walimlilia Bwana Mungu wao awasaidie. Walikuwa wamekata tamaa kutokana na maadui waliokuwa wamewazingira na kuziba kila njia ya kutorokea.
20 Jeshi zima la Waashuru, wanajeshi wapandafarasi, wapanda magari ya farasi na wale wa miguu, liliwazingira Waisraeli kwa muda wa siku thelathini na nne. Maji yalikwisha katika kila chombo cha maji wakazi wa Bethulia walichokuwa nacho.
21 Hata maji waliyohifadhi yalikwisha; hakuna mtu aliyeweza kunywa maji akatuliza kiu kwani waligawiwa kidogokidogo.
22 Watoto walianza kudhoofu; kila mahali mitaani na barabarani mjini, wanawake na vijana wakawa wanazimia. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na nguvu za kumtosha.
23 Ndipo watu wote mjini, wanaume, wanawake na watoto, walipomkusanyikia Uzia akiwa na maofisa wa mji, wakawaambia kwa sauti kubwa,
24 “Mungu atawahukumu kwa yote mliyotutenda. Mmetuletea madhara makubwa kwa kuwa hamkufanya mapatano ya amani na Waashuru.
25 Sasa hatuna yeyote wa kutusaidia! Mungu ametutia mikononi mwao, nasi tutakufa mbele yao kwa kiu na bila msaada.
26 Waiteni mara moja; usalimishe mji utekwe na watu wa Holoferne na majeshi yake.
27 Ni afadhali kwetu kuwa mateka wao kuliko tulivyo sasa, angalau tutakuwa hai bila kuona watoto wetu wachanga wakifa mbele ya macho yetu wala wanawake wetu na watoto wakikata roho.
28 Basi mbingu zishuhudie pamoja na dunia, hata Mungu wetu pia, aliye Bwana wa babu zetu, yeye anayetuadhibu sisi kutokana na dhambi zetu na dhambi za wazee wetu. Tunawaomba mfanye hivyo sasa hivi; leo.”
29 Basi maombolezo ya uchungu yakatokea katika mkutano wote, nao wote wakamlilia Bwana, Mungu wao, kwa sauti kubwa.
30 Kisha Uzia akawaambia, “Msife moyo, ndugu zangu! Tuvumilie kwa muda wa siku tano, mpaka wakati huo Bwana Mungu wetu atakapotuonea huruma; kwani kwa hakika hawezi kututupa kabisa.
31 Lakini ikiwa hata baada ya siku hizo tano hakuna msaada wowote, nitafanya kama mlivyosema.”
32 Halafu Uzia aliwaruhusu watu waende zao. Wanaume wakarudia sehemu zao za ulinzi kwenye minara nao wanawake na watoto wakarudi nyumbani. Mji ulikuwa na hali ya kukatisha tamaa kabisa.

Generic placeholder image