8

Yudithi, mwanamke Mwisraeli mjane
1 Wakati huo, Yudithi alisikia mambo yaliyotokea. Yeye alikuwa binti wa Merari, mwana wa Oksi, mwana wa Yosefu, mwana wa Ozieli, mwana wa Elkia, mwana wa Anania, mwana wa Gideoni, mwana wa Refaimu, mwana wa Ahitubu, mwana wa Elia, mwana wa Hilkia, mwana wa Eliabu, mwana wa Nathanaeli, mwana wa Salamieli, mwana wa Sarasadai, mwana wa Israeli.
2 Manase, mume wa Yudithi, ambaye alikuwa wa kabila la mkewe na wa ukoo mmoja, alikuwa amefariki wakati wa mavuno ya shayiri.
3 Alikuwa amepigwa sana na jua alipokuwa shambani akisimamia wafanyakazi wakifunga miganda. Baadaye alikwenda akalala kitandani. Halafu alifia katika mji wake Bethulia. Alizikwa katika kaburi la ukoo wake, kati ya mji wa Dothani na mji wa Balamoni.
4 Kwa muda wa miaka mitatu na miezi minne, Yudithi aliishi akiwa mjane.
5 Katika muda huo wa huzuni, yeye mwenyewe alipiga hema darini mwa nyumba yake na kukaa humo, amefunga kiunoni mavazi ya gunia na kuvaa mavazi ya ujane. 6Katika muda huo wote wa ujane wake, alifunga, isipokuwa jioni ya kuanza Sabato, Sabato yenyewe, jioni ya sikukuu ya mwezi mwandamo na sikukuu yenyewe, pamoja na sikukuu zote na siku za mapumziko ambazo Waisraeli waliziadhimisha. 7Yudithi alikuwa mwanamke mzuri sana. Marehemu Manase, mumewe, alikuwa amemwachia dhahabu, fedha, watumishi na watumwa wa kiume na kike, mifugo na shamba na alitunza mali yake yote. 8Hakuna mtu aliyekuwa na neno dhidi yake, kwani alimcha Mungu kwa dhati.

Yudithi anakutana na maofisa wa mji
9 Yudithi aliposikia maji yalivyowafanya watu wateseke na jinsi walivyokuwa wanalalamika vikali dhidi ya viongozi wa mji na jinsi Uzia alivyowaambia na kuwaapia kutoa mji kwa Waashuru baada ya siku tano,
10 Yudithi alimtuma mara moja mjakazi wake aliyekuwa mkuu nyumbani mwake, ili kuwaita Kabrisi, Karmisi na wazee wa mji.
11 Walipomjia, Yudithi aliwaambia, “Nisikilizeni viongozi wa Bethulia. Mlikosea kuzungumza na watu kama mlivyofanya leo na kujifunga kwa kiapo, kwa kumwasi Mungu, kusalimisha mji kwa maadui zetu ikiwa Bwana hakuwapatia msaada katika muda huo uliopangwa.
12 Nyinyi ni nani hata kumjaribu Mungu kama mlivyofanya leo, na kujitia mahali pa Mungu kuhusu mambo ya watu?
13 Mnamjaribu Bwana Mwenye Nguvu! Hamfahamu lolote, wala hamtafahamu.
14 Kama hamwezi kuyafahamu yaliyo moyoni mwa mwanaadamu, wala anayofikiri, mnawezaje basi, kufahamu akili ya Mungu aliyeumba vitu vyote au kuyaelewa mawazo yake au makusudi yake? Sivyo hivyo ndugu! Msimkasirishe Bwana Mungu wetu!
15 Ikiwa hataki kutusaidia katika muda huu wa siku tano, bado anaweza kutukinga na hatari kwa siku nyingi jinsi yeye apendavyo, kama alivyo na uwezo wa kutuangamiza mbele ya maadui zetu.
16 Hamna haki ya kudai uhakikisho pale mipango ya Mungu inapohusika. Mungu hastahili kutishwa wala hapaswi kufanyiwa mzaha, kama mwanaadamu wa kawaida.
17 Zaidi ya hayo! Kama tumngojeavyo atukomboe, basi tumsihi atusaidie; ikiwa hayo ni mapenzi yake, atakisikiliza kilio chetu.
18 Kamwe katika nyakati zetu hizi na hata leo; hakuna kabila moja miongoni mwa makabila yetu au jamaa au kijiji kinachoiabudu miungu iliyofanywa kwa mikono ya mwanadamu, kama hapo awali.
19 Ndiyo maana wazee wetu waliachwa wauawe kwa upanga na kutekwa, halafu waliangamia katika taabu kwa kushambuliwa na maadui zetu.
20 Sisi kwa upande wetu hatumwabudu mungu yeyote mwingine bali yeye; kwa hiyo tuwe na tumaini kuwa hatatuchukia wala kulitupilia mbali taifa letu.
21 “Ikiwa kweli watatuteka, basi, eneo zima la Yudea litatekwa pia, hata mahali petu patakatifu patabomolewa, nasi tutalipa kwa damu yetu kwa ajili ya tendo lao la kufuru.
22 Kuuawa kwa ndugu zetu, kutekwa kwa nchi yetu, na kuangamizwa urithi wetu vitakuwa lawama yetu wenyewe kati ya mataifa tutakaokuwa watumwa wao; nao mabwana zetu wapya watatudharau kama taifa ovu na lenye hila.
23 Hakuna jema litakalopatikana kutokana na utumwa wetu, bali Bwana Mungu wetu ataufanya kuwa jambo la aibu.
24 “Sasa ndugu zangu, ni lazima sisi tuwe mfano kwa ndugu zetu, maana maisha yao yanatutegemea sisi, kadhalika mahali patakatifu: Hekalu na madhabahu ni juu yetu kuvitunza.
25 Zaidi ya hayo yatupasa kumshukuru Bwana Mungu wetu ambaye kama alivyowajaribu wazee wetu ndivyo anavyotujaribu.
26 Kumbukeni jinsi alivyomtendea Abrahamu majaribu yote kuhusu Isaka, na yale yaliyompata Yakobo alipomtumikia Labani, mjomba wake, katika nchi ya Mesopotamia ya Siria.
27 Maana kama majaribu hayo yalikusudiwa na Mungu ili kuchunguza mioyo yao, hivyo basi hiki si kisasi ambacho Mungu anatulipiza, bali, ni onyo ambalo limepelekwa na Bwana kwa wale anaowapenda.”
28 Kisha Uzia alimwambia Yudithi, “Yote uliyosema yanatokana na moyo safi, na hakuna awezaye kupinga neno lolote.
29 Leo si mara ya kwanza kwako kutuonesha hekima yako. Tangu utoto wako, sisi tumetambua ulivyo mwenye akili na moyo thabiti.
30 Lakini kwa ajili ya kuona kiu sana watu wetu walitushurutisha kufanya kama tulivyowaahidi na kujifunga kwa kiapo halisi.
31 Wewe ni mcha Mungu sana, mwombe Bwana atuletee mvua ili visima vyetu viwe na maji, ili kuangamia kwetu kukome.”
32 Basi, Yudithi akawaambia, “Nisikilizeni, ninakusudia kutenda jambo ambalo litakumbukwa katika vizazi vyote vya wazawa wetu.
33 Leo usiku, shika ulinzi kwenye lango la mji. Mimi na mjakazi wangu tutatoka mjini. Kabla haijafika siku ile ambayo umeahidi kusalimisha mji wetu kwa maadui zetu haijafika, Bwana atanitumia mimi kuwaokoa Waisraeli.
34 Lakini msiniulize ninalokusudia kutenda; sitawaambieni mpaka nitakapolitenda.”
35 Uzia pamoja na wakuu wakamwambia, “Nenda kwa amani! Bwana Mungu akuongoze kuwalipiza kisasi maadui zetu”.
36 Hivyo, wakaondoka kutoka kwenye kibanda kilichokuwa darini, wakarudi kwao.

Generic placeholder image