6

Hotuba ya Holoferne
1 Baada ya ghasia zilizosababishwa na Akioro kwenye mkutano kutulia, Holoferne, jemadari wa jeshi la Ashuru, alimwambia Akioro, mbele ya wanajeshi wote wa kukodishwa kutoka pwani ya bahari ya Mediteranea na Wamoabu.
2 “Akioro, wewe ni nani, na wanajeshi wa kukodishwa kutoka Efraimu, hata ujifanye nabii? Wewe ni nani kututabiria tusiende kupigana na watu wa Israeli ati kwa sababu Mungu wao atawalinda? Ni nani aliye mungu kama si Nebukadneza?
3 Nebukadneza atapeleka wanajeshi wake na kuwatupilia mbali watu hao kutoka uso wa dunia. Mungu wao hataweza kuwaokoa. Sisi ambao ndio watumishi wa mfalme Nebukadneza tutawaangamiza mara moja. Hawawezi kusimama dhidi ya nguvu za jeshi letu.
4 Tutawateketeza mara moja, milima yao itafurika damu yao na mashamba yao yatajaa maiti. Hawawezi kushindana na sisi. Mfalme Nebukadneza, bwana wa dunia yote ameagiza kuwa ni lazima kuwafagilia mbali, na maneno aliyoyasema hayawezi kuwa yasiyo na maana.
5 “Lakini wewe Akioro uliyekodishwa na Waamoni, wewe ni msaliti. Hutaniona tena hadi hapo nitakapokuwa nimewaadhibu wale watoro kutoka nchi ya Misri.
6 Baada ya hayo, wanajeshi wangu watakuua kwa upanga. Utakuwa mmoja wao wale watakaouawa.
7 “Sasa, watu wangu watakupeleka milimani na kukuacha katika mmojawapo wa miji ya watu wa Israeli,
8 nawe utafia huko pamoja na watu wengine.
9 Usiwe na masikitiko ikiwa unafikiri kuwa hawatashindwa. Nimesema, hakuna neno langu lolote litakalokuwa halina maana.”

Akioro anapelekwa mjini Bethulia
10 Basi, Holoferne akawaagiza watu wake waliokuwa wanamtumikia kwenye hema yake wamkamate Akioro na kumpeleka mjini Bethulia, wakamkabidhi kwa watu wa Israeli.
11 Wale watu wakamkamata Akioro, wakamtoa nje ya kambi na kumpeleka bondeni. Kutoka huko wakampeleka milimani kwenye chemchemi iliyokuwa karibu na mji wa Bethulia.
12 Watu wa mjini walipowaona wale watu wanakaribia mjini, wakachukua silaha zao na kukimbilia mlimani. Kila mtu aliyetumia kombeo kama silaha akawa anawarushia mawe wanajeshi wa Holoferne. Hivyo, hao wanajeshi wakashindwa kupanda mlimani.
13 Wakalazimika kujikinga ubavuni mwa mlima, ambapo walimfunga Akioro kamba. Kisha wakamwacha hapo, wakaenda zao kwa mkuu wao.
14 Baadaye, Waisraeli waliposhuka kutoka mjini Bethulia walimfungua Akioro, wakampeleka mjini kwa maofisa wa mji.
15 Wakuu wa wakati huo walikuwa Uzia, mwana wa Mika, kutoka kabila la Simeoni, Kabrisi mwana wa Gothonieli, na Karmisi mwana wa Melkieli.
16 Hao maofisa wakawakusanya wazee wa mji, nao wanawake wote na vijana wakakimbilia mkutanoni. Akioro akaletwa mbele ya watu, na Uzia akaanza kumhoji.
17 Akioro akawasimulia yote yaliyosemwa kwenye mkutano wa Holoferne kuhusu vita. Akawasimulia yale aliyosema yeye mwenyewe mbele ya viongozi wa Waashuru na jinsi Holoferne alivyojigamba angewatenda watu wa Israeli.
18 Watu waliposikia hayo, walianguka chini na kumwabudu Mungu. Wakamlilia wakisema,
19 “Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, ona jinsi maadui zetu wanavyojigamba na jinsi wanavyokusudia kutudhili. Tuonee huruma sisi watu wako”.
20 Kisha, wakamthibitishia Akioro juu ya usalama wake na kumsifu sana kwa yote aliyotenda.
21 Baada ya mkutano kumalizika, Uzia akampeleka Akioro nyumbani kwake ambako alimfanyia karamu pamoja na wazee wa mji. Usiku kucha wakamwomba Mungu wa Israeli awasaidie.

Generic placeholder image