70

Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi ya matoleo ya ukumbusho)
1 Upende kuniokoa ee Mungu! Ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia.
2 Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika.
3 Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao.
4 Lakini wote wale wanaokutafuta, wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mungu ni mkuu!”
5 Nami niliye maskini na fukara, unijie haraka, ee Mungu! Ndiwe msaada wangu na mkombozi wangu; ee Mwenyezi-Mungu, usikawie!

Generic placeholder image